Mafunzo ya Kuanzisha Biashara Ndogondogo.
Lemburis Kivuyo Katika Mafunzo ya Kuanzisha Biashara Ndogondogo

Hatua 26 za Kufuata Katika Kuanzisha Biashara Ndogondogo

Zifuatazo ni hatua 26 za kufuata katika kuanzisha biashara ndogondogo. Zitamuwezesha mtu yeyote kuanzisha biashara yeyote kwa uraisi zaidi.

Hatua ya kwanza YA KUAMUA ikiwa imebeba hatua zingine zote kwani biashara inahitaji utayari (maamuzi tena saa nyingine MAAMUZI MAGUMU) zaidi ya vitu vingine kama mtaji nk

Hatua ya ya 1: Kuamua kuingia katika biashara

Kuamua kuingia katika biashara ni mjumuisho wa utayari wa kisaikolojia, kiakili, kiuchumi, kiimani ili kuweza kukabiliana na hatari au vitisho vyote vitakavyojitokeza kwenye biashara.

Maamuzi yako na hasa maamuzi magumu juu ya aidha kufanya hiyo biashara au la si ile hali ya kuamua kufanya biashara tu, bali pia ni ile hali ya kukubaliana na ups and downs za biashara husika na kuwa tayari kujitoa mhanga zaidi.

Hatua ya 2: Kuchanganua uwezo na udhaifu wako

Uwezo wako katika kutekeleza biashara husika ni muhimu sana. Kila mtu anao uwezo fulani katika maisha yake ila sio wote tunaojua ni uwezo gani tunao kwa manufaa gani na kwa wakati gani. Ni vyema sasa kuchambua uwezo wako wote ili kuangalia ni namna gani, wapi, lini unaweza kuutumia uwezo huo katika kuleta tija ya biashara yako. Kila mtu pia ana madhaifu tena mengi tu. Udhaifu ukiendekezwa unaweza angamiza kabisa biashara yako. Kwa hiyo ni muhimu kujua kwa kuorodhesha madhaifu yote uliyonayo ili uweze kuyapatia dawa kabla hayakuleta madhara kwenye biashara yako.

Maeneo manne ni muhimu yapatiwe taarifa halisi na kuchukua hatua ili uweze kumudu kufanya biashara husika.

Maeneo hayo ni

  1. Uwezo wako (Hupatikana kwenye mazingira ya ndani na wezeshi)
  2. Udhaifu wako (Hupatikana kwenye mazingira ya ndani na pingamizi)
  3. Fursa zilizopo  (Hupatikana kwenye mazingira ya nje na wezeshi)
  4. Hatari zilizopo (Hupatikana kwenye mazingira ya nje na pingamizi)

Tafsiri

  • mazingira ya ndani ni yale mambo yote (udhaifu na uwezo) ambayo mhusika anaweza kuyabadili
  • mazingira ya nje ni yale mambo yote (fursa na hatari) ambayo mhusika hawezi kuyabadili
  • mazingira wezeshi ni yale mambo yote (fursa na uwezo) ambayo zikiwepo biashara yako itanufaika kwa kuimarika
  • mazingira pingamizi ni yale mambo yote (udhaifu na hatari) ambayo zikiwepo biashara yako inaweza kufa

Maeneo ya kuchambua kwenye jedwali kwa ufupi

Mazingira wezeshi Mazingira pingamizi
Mazingira ya Ndani Uwezo:  Uwezo wako katika kuendesha biashara mfano: utaalam, vitendea kazi, kiwanja nk. Udhaifu:  Udhaifu wako katika kuendesha biashara mfano: ukosefu wa utaalam, vitendea kazi, kiwanja nk.
Mazingira ya Nje Fursa:  Kuwepo kwa sera nzuri, katiba nzuri, hali ya hewa nzuri, mwitikio wa jamii nk Vitisho:  Kutokuwepo kwa sera nzuri, katiba nzuri, hali ya hewa nzuri, mwitikio mbaya wa jamii nk

Hatua ya 3: Kupata mafunzo

Baada ya kujua udhaifu wako, pata mafunzo ili udhaifu wako usiadhiri biashara yako

Mfano:-

  • Kupata mafunzo ya ufundi fulani mfano namna ya kutengeneza sabuni ya maji nk
  • Kupata elimu ya kubadili mitizamo mbaya juu ya mambo muhimu kwenye biashara yako. mfano mtizamo wa kwamba wewe huwezi kufanya biashara ikafanikiwa nl

Hatua ya 4: Kupeleleza mazingira utakayofanya biashara

Ni lazima upeleleze ili ujue fursa na hatari zilizopo katika biashara hiyo. mfano hatari (Risks, constraints) zaweza kuwa ni sheria na sera mbaya za nchi, sheria na sera kandamizi za kimataifa, barabara mbovu, hali ya hewa mbovu nk. Unatakiwa kusijua zote hizo ili aidha uweze kuzikwepa au kuzikabili.

Fursa nzuri zilizopo zaweza kuwa ni sheria na sera nzuri, miundo mbinu nzuri, udongo wa rutuba na mvua za kutosha kila mwaka nk

Hatua ya 5: Kuchagua biashara gani ufanye

i)    Kuzalisha bidhaa (Manufacturing)

ii)   Kuchuuza (Kuuza bidhaa)

iii)  Kutoa huduma (Service)

Kuzalisha bidhaa

Kuzalisha bidhaa ni kutumia rasilimali watu na malighafi ili kutengeneza bidhaa ya kuuza kwa mlaji au mchuuzi. Bidhaa ni kama vyakula, vyombo, nk

Kuuza bidhaa (Trading)

Kuchuuza bidhaa zilizotengenezwa na wengine ili kupata faida. Unaweza uza moja kwa moja kwa mlaji au ukauza kwa jumla (whole sale)

Kutoa huduma (Service)

Kutumia ujuzi wako au wa wengine katika kuwahudumia watu na shida zao kwa malipo. Mfano kufundisha, kutibu, kusafirisha, kutumbuiza nk

Hatua ya 6: Utafiti wa soko (Market Survey)

Utafiti wa soko ni muhimu ufanyike ili kuwajua washindani wako katika biashara husika. unatakiwa kupeleleza uwezo na udhaifu wao nk

Peleleza pia yafuatayo

  • Washindani wakubwa wako wangapi – uwezo wao ni upi na udhaifu wao ni upi?
  • Ukubwa wa soko
  • Mgawanyo wa soko
  • Aina ya soko/masoko
  • Tabia za soko
  • NK

Hatua ya 7: Kuchagua mfumo gani wa biashara utumie

Fuatilia maelezo ya kila mfumo ukitilia maanani faida na hasara za kila mfumo. Unaweza pia kumtumia mshauri wa masuala ya biashara kukushauri kulingana na mazingira yako utakayofanyia biashara.

Hasa unatakiwa kujua zaidi mambo ya kisheria katika mfumo utakaoamua kuutumia kuendehsa baishara yako ili isije ikakuletea shida huko mbeleni, maamuzi ya mfumo upi uuchukue inategemea zaidi sheria za ndani ya nchi husika, pia inategemea ukubwa wa mtaji wako nk.

Mtu mmoja (sole proprietor)

Hii ni biashara inayoendeshwa na mtu mmoja tu kwa kutumia jina lake binafsi au kusajili brela jina la biashara tofauti na jina lake inafsi

Faida yake

  • Kuanzisha ni rahisi
  • Maamuzi hupitishwa kwa haraka kwa hiyo hakuna urasimu

Hasara yake

  • Biashara ikipata shida mmiliki anahusika na hasara kama vile ya ufilisi nk
  • Yaani biashara ikidaiwa mali za mmiliki kama nyumba, gari, shamba zitauzwa ili kulipa madeni

Ushirika au Partnership (watu wawili kwenda juu)

Hii ni biashara inayoendeshwa na watu wawili au zaidi kwa mfumo ule ule wa mtu mmoja lakini hapa ni lazima kusajili jina la biashara brela na kuandika mkataba wa ushirika yaani Partnership Agreement

Faida yake

  • Kuanzisha ni rahisi
  • Maamuzi hupitishwa kwa haraka kwa hiyo hakuna urasimu japo sio kama biashara ya mtu mmoja

Hasara yake

  • Biashara ikipata shida wamiliki wanahusika na hasara kama vile ya ufilisi nk
  • Yaani biashara ikidaiwa mali za wamiliki kama nyumba, gari, shamba zitauzwa ili kulipa madeni
  • Mikataba inayoingiwa na mmoja wa washirika huwabana na wengine wasiohusika

Kampuni ya umma (public companies)(zaidi ya watu wawili bila ukomo)

Kampuni za uma ni zile zinazoitwa kwa kiingereza Public Limited Companies by Share au kwa kifupi PLC. Hizi kampuni zinakuwa na wanahisa bila ukomo na hisa zake huwa zinauzwa kwenye masoko ya hisa kwa uwazi bila siri. Biashara zake husimamiwa na utawala ambao mkurugenzi wake huchaguliwa na bodi ya wakurugenzi ambao hasa ndio wamiliki wa kampuni kwa niaba ya wana hisa wote.

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio wenye hisa
  • Ni rahisi kuvutia mitaji mikubwa kupitia masoko ya hisa

Hasara yake

  • Haina usiri hivyo ni hatari kwani washindani wa biashara husika wanaweza kutumia taarifa hizo kujipanga
  • Rasilimali muda na pesa kupotea kwa shughuli za ndefu za kihasibu, kisheria na za kodi za serikali. Kwa ufupi paper work ni kubwa, inafuatiliwa sana na TRA, BRELA na taasisi mbalimbali za udhibiti na uhakiki

Kampuni ya binafsi yenye ukomo wa hisa

Kampuni za binafsi ni zile zinazoitwa kwa kiingereza Private Limited Companies by Share. Hizi kampuni zinakuwa na wanahisa kuanzia wawili mpaka 50 na hisa zake haziruhusiwi kuuzwa kwenye masoko ya hisa au kwa uwazi wa aina yeyote. Biashara zake husimamiwa na utawala ambao mkurugenzi wake huchaguliwa na bodi ya wakurugenzi ambao hasa ndio wamiliki wa kampuni kwa niaba ya wana hisa wote.

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio wenye hisa
  • Kazi za makaratasi ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
  • Mlolongo wa taratibu za kisheria ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma

Hasara yake

  • Gharama katika kuanzisha tofauti na biashara binafsi
  • Huruhusiwi kuuza hisa katika masoko ya hisa
  • Kampuni li lazima angalau iwe na wakurugenzi, katibu na mhasibu
  • Ni lazima ifanyiwe ukaguzi wa mahesabu kila mwaka

Kampuni ya binafsi yenye ukomo wa udhamini

(private companies limited by guarantees) (watu wawili hadi 50)

Kampuni hizi hufanana na zile za binafsi isipokuwa kampuni binafsi zenye ukomo wa udhamini huwa ni kampuni zisizo za faida na kwa hiyo wadhamini wake hawaruhusiwi kugawana faida. Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali hasa yale ya uwanaharakati zinaanzishwa kwa kutumia mfumo huu badala ya ule wa NGO au CBO kwa sababu za usalama wa kisheria. Mashirika yalisajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa wa udhamini zinalindwa na sheria za usajili wa makampuni ambayo wanasiasa hawawezi kufuta kampuni hata kama inaendesha harakati zinazoichukiza serikali.

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio kwa wadhamini
  • Kazi za makaratasi ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
  • Mlolongo wa taratibu za kisheria ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma

Hasara yake

  • Gharama katika kuanzisha tofauti na biashara binafsi
  • Kampuni li lazima angalau iwe na wakurugenzi, katibu na mhasibu
  • Ni lazima ifanyiwe ukaguzi wa mahesabu kila mwaka

Jumuiya (association)

Jumuiya ni muungano wa watu au taasisi zenye lengo moja lizilo la kiserikali au kibiashara

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Inavutia wahisani
  • Ni ya watu wachache waliokubaliana

Hasara yake

  • Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
  • Ugomvi wa mara kwa mara
  • Haina kinga kwa waazilishi ukilinganisha na makampuni

Vyama vya ushirika

Vyama vya ushirika ni muunganiko wa aidha wafanyakazi au wakulima kwa lengo la kukuza umiliki katika maeneo yao ya kazi au masoko ya biashara

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Inavutia wahisani
  • Ni ya watu wachache waliokubaliana

Hasara yake

  • Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
  • Ugomvi wa mara kwa mara
  • Haina kinga kwa waazilishi ukilinganisha na makampuni
  • Mashirika yasiyo ya kiserikali

Bodi ya wadhamini (Board of Trustee)

Faida yake

  • Utambulisho wa kisheria
  • Inavutia wahisani
  • Ni ya watu wachache waliokubaliana

Hasara yake

  • Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
  • Ugomvi wa mara kwa mara
  • Haina kinga kwa waazilishi ukilinganisha na makampuni

Ukishachagua mfumo mzuri wa biashara yako, unatakiwa kuanza mchakato wa kuisajili katika mamlaka ya usajili wa makampuni inayoitwa BRELA ambayo ofisi zake zipo Jengo la shirika –Dar es salaam

Hatua ya 8: Kuchagua sehemu ya biashara

Kama ni sheli itabidi iwekwe kando ya barabara yenye magari mengi

Hatua ya 9: Kuchagua teknolojia

Ni muhimu kuangalia, kama biashara yako inategemea kwa ukubwa wake teknolojia usiende haraka hapa, tumia wataalamu wa technolojia husika ujua pro and cons zake kwani ukiharakisha hapa utaingia gharama isiyotakiwa na kuibebesha biashara yako mzigo wa manunuzi ambao hazikutakiwa, lakini pia technolojia husika inaweza kuchangia katika kupata faidi kubwa au hasra kubwa. uwe makini hapa.

Teknolojia itasaidia kujua

a)    Aina ya  watumishi

b)   Aina ya vitendea kazi mashine  /mitambo

Mfano kilimo cha maksai na kukamua kwa mashine

Teknolojia nzuri ni lazima iwe na sifa zifuatazo

a)    Ni rahisi kutumiwa

b)   Iwe rahisi kupata msaada kama mafundi nk

c)    Iwe inaendana na tamaduni husika

d)   Iwe ni rafiki wa watu na mazingira

e)    Iwe na gharama ndogo za uendeshaji

f)     Inaendelezeka

Hatua ya10: Kununua mashine na vifaa

Mashine na mitambo mingine itategemea sana uchaguzi wa teknolojia hapo juu 8(i)

Mashine zote na mitambo ni lazima kuzingatia yaliyotajwa hapo juu 8(ii)

Hatua ya 11: Usajili wa biashara

Hii hufanywa mara nyingi kwenye manispaa husika. Hakikisha pia unasajili biashara yako kwenye idara au mamlaka husika ya serikali inayodhibiti biashara kama yako.

mfano

  • Biashara ya vyakula au madawa – mamlaka ya vyakula na madawa -TFDA
  • Biashara ya shule – idara ya elimu au wizara ya elimu nk

Hatua ya 12: Kuandika Mchanganuo wa Biashara (Business Plan)

  • Baada ya kufanya hayo yote sasa ni wakati mzuri wa kuandika  mchanganuo wa biashara yako
  • Mchanganuo wa biashara ni maelezo ya kina ambayo inaonyesha biashara yako ilikotoka, inakokwenda, hali ya masoko, sekta, kifedha na uongozi wa biahara yako. Ni taarifa muhimu ya kuwavutia wawekezaji na watoa mikopo kama mabenki

Mambo muhimu ya kujua katika kuandika Mchanganuo wa Biashara

1. Kasha la nje

2. Maelezo wa biashara yako

3. Historia na maelezo ya biashara yako

4. Maelezo ya bidhaa au huduma ya biashara yako

5. Mchanganuo wa masoko

  • Washiriki, uwezo an madhaifu yao
  • Ukubwa wa soko
  • Mgawanyo wa soko
  • Aina ya soko/masoko

6.  Mkakati wa utekelezaji

  • Uongozi na usimamizi wa kazi
  • Uchambuzi wa madhaifu, nguvu, fursa na hatari zinazokabili biashara yako
  • Mkakati wa Uzalishaji
  • Mkakati wa kuuza

7.  Mpango wa fedha

  • Uchambuzi wa mahitaji ya mtaji
  • Wapi utatoa mtaji
  • Matumizi ya mtaji
  • Makisio ya Mauzo
  • Uchambuzi wa kurudisha gharama (break even analysis)
  • Makisio ya faida au hasara
  • Makisio ya mzunguko wa fedha katika biashara yako (cashflow)
  • Makisio ya oanisho la mali na madeni ya biashara yako (balance sheet)
  • Ulinganifu wa sehemu mbalimbali za biashara (business ratios)

8.  Viambatanisho

  1. Lesseni
  2. Cheti cha ulipaji kodi
  3. TIN
  4. Cheti cha usajili
  5. Mikataba
  6. Risiti za manunuzi hasa mali za Biashara
  7. Taarifa zingine ambazo hazikupata nafasi ndani ya mchanganuo huu
  8. Taarifa zingine zinazoweza kuifanya biashara au kampuni kuaminika zaidi

Hatua ya 13: Kupanga juu ya pesa.

Kutafuta mikopo kwa kufuata utaratibu wa taasisi za fedha husika

Taasisi nyingi huhitaji yafuatayo

  1. Dhamana ya mkopo
  2. Uzoefu wa biashara husika
  3. Mchanganuo wa biashara
  4. Maombi ya mkopo

Hatua ya 14: Ufahamu wa kiufundi.

Hii ifanywe ili mwenye biashara apate ufahamu wa kiufundi juu ya biashara yake hasa kutoka kwa taasisi husika au mshauri wa biashara (consultant).

Hatua ya 15: Kujua vyanzo vya nishati:

Kama ni umeme hakikisha iko sawa na umeme utakidhi matakwa ya biashara.

Kama ni mafuta uhakikishe mafuta inapatikana na bei haitaadhiri bei ya bidhaa

Hatua ya 16: Kuweka vifaa: (Machines installation)

Wataalam husika wafanye hii kazi

Hatua ya 17: Kuajiri wafanyakazi.

Wafanyakazi wako wengi mtaani, lakini kumpata mtu atakayekidhi matakwa ya biashara yako kwa maana ya ubora na kufikia lengo la uzalishaji inahitaji usambazaji wa taarifa kwa upana zaidi na kwa maeneo maalum ambayo unategemea wafanyakazi watoke. Mfano vyuoni, makanisani nk

Unashauriwa pia kutumia marafiki na ndugu wa karibu ili upate mfanyakazi ambaye ni bora zaidi

Hatua ya 18: Kujua upatikanaji wa malighafi/biadha/huduma

Kama unazalisha malighafi bila ubishi ni kiungo muhimu kwa biashara yeyote inayohusisha kuzalisha bidhaa. Vivyo hivyo kama unachuuza, sehemu ya kupata bidhaa kwa bei ya jumla ni muhimu uzijue na kuziweka kwenye database yako. Na pia kama wewe ni mto huduma, unatakiwa kujua utapata wapi huduma zitakazokuwezesha wewe kuwahudumia wateja wako vizuri.  Vyanzo vya kupata malighafi/bidhaa/huduma ni muhimu ijulikane na iwe ya uhakika.

Hatua ya 19: Uzalishaji mali

  • Uzalishaji wa majaribio , Kuuza kwa majaribio kutoa huduma kwa majaribio muda – miezi 2-6, nk
  • Kuanza biashara rasmi
  • Kutunza siri ya unavyozalisha au kutoa huduma tofauti na wengine
  • Tunza vizuri siri zingine za biashara yako

Hatua ya 20: Kuhakikisha bidhaa yako hainakiliki

  • Kama unatengeneza biadhaa hakikisha fomula na mbinu ulizotumia ni ngumu na zimefanywa siri kubwa
  • Pia hakikisha unalinda hati miliki ya huduma au bidhaa husika katika ngazi husika za usajili na utambuzi

Hatua ya 21: Usalama wa biashara yako

Epuka majengo ambayo ni rahisi kuwaka moto, kubomolewa na wezi, wizi katika pesa za mauzo, utapeli wa bidhaa katika kununua na kuuza nk.

Hatua ya 22: Kuuza (Selling)

Kufikia wateja (fikiria utamfikiaje mteja wako wa kwanza – maelezo zaidi yatakuwepo katika mchanganuo wa biashara)

  • Kusambasa huduma/bidhaa
  • Kuweka bei
  • Kutangazia biashara
  • Promosheni nk.

Hatua ya 23: Utafiti wa soko (Market Research)

 

  • Hii ifanywe kila mara ili kujua kama wateja wamebadilika au bado Ili kujua kama wanapenda huduma/bidhaa zako au la.
  • Kujua biashara yako imekamata asilimia gani katika soko
  • Kupata maoni ya wateja ili kuboresha biashara/huduma/bidhaa

Namna ya kufanya utafiti

 

Utafiti wa kuendelea

Kila mteja anaponunua bidhaa, ajaze fomu maalum ya maoni. Mfano ya jinsi alivyohudumiwa, bei ya bidhaa, usindikaji, ubora nk

Utafiti maalum

Huu ufanywe wakati wa kutoa vivutiuo maalum au promosheni maalum.

Mteja wa promosheni ajaze fomu maalum ya maoni. Mfano ya jinsi alivyohudumiwa, bei ya bidhaa, usindikaji, ubora nk

Hatua ya 24: Kusimamia na kuthibiti biashara

Hii ni kuhakikisha kuwa biashara inakwenda kama ilivyobuniwa /pangwa. weka mifumo ya kudhibiti na kuhakikisha ubora unafikiwa nk

Hatua ya 25: Kutathmini biashara

Hii ni kujua kama biashara imekwenda kama ilivyobuniwa /pangwa.

Mambo ya kuangalia

  1. Mapato na matumizi
  2. Bajeti iliyopita
  3. Matokeo ya utaifit/wa soko

Hatua ya 26: Kufanya maboresho/mabadiliko

Unaweza kumuajiri au kumtumia mtaalam wa sekta hiyo kufanya taadhmini ya biashara yako.

Fanya sawa sawa na matokeo ya tathmini/utafiti

 

Mwisho (End):

Kama umependa makala hii weka maoni yako ya shukrani hapo chini au washirikishe marafiki zako wa kwenye Facebook, Instagram, Linkedin, Whatsapp, Twitter na kwenye email au mitandao mingine ya kijamii. Wasiliana nasi kama unataka kuweka kwenye blogu au website yako kwa maelekezo zaidi

If you found this article helpful please leave the comment below or share to your friends in Facebook, Instagram, Linkedin, Whatsapp, Twitter and in email or other social media. Contact us if you plan to list in your blog or website for further instructions.

Tutembelee kwenye mitandao ya kijamii hapa chini:

We offer but not limited to the following:
Business Office Documents Development, Company Registration, Business Plan Development, Curricula Development for colleges, Office Digitization Consultancy, Online Presence and Marketing Consultancy, Leadership and Management Consultancy, Constitution Development  and much more

English Form

Fomu ya Kiswahili


city, country
mji, nchi